Thursday, November 26, 2020

SINGIDA YAWANOA WANAUSHIRIKA

 

Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Singida, Thomas Nyamba akiongea na Waandishi wa Habari.

                  

Mwenyekiti wa   Chama Kikuu Cha Ushirika  cha Wakulima Mkoa wa Singida (SIFACU LTD) Yahaya Ramadhani  akiongea na Waandishi wa Habari


 Wajumbe wa Bodi na Watendaji wa   Vyama vya Ushirika  katika  Mkoa Singida  wakipewa mafunzo

                            ......................................

 

John Mapepele na Rose Nyangasa, Singida

Mkoa wa Singida umeandaa  mafunzo  ya siku  tatu ya kuwajengea uwezo Wajumbe wa Bodi na Watendaji wa   Vyama vya Ushirika  katika  Mkoa ili kuwasaidia  kuacha  kufanya kazi kwa  mazoea  badala yake wafanye  kazi  kwa weledi na kwa kuzingatia sheria  huku wakitanguliza mbele maslahi ya wakulima. 

 

Akifungua mafunzo hayo leo mjini Singida kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia eneo la Uchumi Beatus Choaji amesema Mkoa umeamua kufanya  mafunzo hayo kutokana na kupata taarifa  ya ukaguzi uliofanywa kwenye vyama vya ushirika  kushindwa kufanya vizuri.

 

Choaji amesema Serikali ya Awamu ya Tano ipo macho kwa viongozi wa Vyama Vya Ushirika na maafisa wengine wa Serikali ambao wamekuwa wakishirikiana na walanguzi kuwanyonya wakulima ambapo amesema hili ni  kosa kisheria  na  kuwaonya kwamba  katika kipindi cha sasa Sheria kali zitachukuliwa dhidi yao ikiwa ni pamoja na kuwatia hatiani kwa Sheria ya Uhujumu Uchumi.

 

 “Nawaagiza Watumishi wa Serikali kuacha kufanya kazi kwa mazoea badala yake fanyeni kazi kwa weledi na kuzingatia Sheria huku mkitanguliza mbele maslahi ya wakulima”aliongeza Choaji

 

Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Singida, Thomas Nyamba amesema lengo la  kuandaa mafunzo hayo ni kutoa elimu  ya kuwawezesha Watendaji ili waweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu.

 

Nyamba amesema kumekuwa na makosa mbambali ya kiuzembe  na kitaaluma katika utendaji wa kazi lakini kupitia mafunzo haya watendaji wote watabadilika.

 

Mwenyekiti wa   Chama Kikuu Cha Ushirika  cha Wakulima Mkoa wa Singida (SIFACU LTD) Yahaya Ramadhani  amesema pamoja na mambo mengine wajumbe wa kikao hicho watafundishwa masomo ya uandishi wa vitabu vya mwanzo na vitabu vikuu,uaandaaji wa taarifa za fedha,uongozi na utawala pia na Sheria ya Vyama Vya Ushirika Na.6. ya Mwaka 2013

 

Ameyataja masomo mengine yatakayo fundishwa kuwa ni uandaaji wamakisio ya mapato na matuminzi,uandaaji wa mpango mkakati, utatuzi wa migogoro na usimamizi wa fedha na udhibiti wa rushwa katika vyama vya ushirika.

 

Baadhi ya washiriki katika wa mafunzo hayo wamepongeza juhudi za Serikali ya awamu ya Tano kutoa mafunzo na kusema kwamba yataongeza tija katika utendaji wao wa kazi.

 

Mwenyekiti wa AMCOS wa Wilaya ya Ikungi Mnang’ana Rukia Jumanne amesema mafunzo hayo yamewasaidia kutambua majukumu ya kila mmoja kwenye vyama vya ushirika hivyo yatawawezesha kufanya kazi bila kuingiliana nakwa weledi tofauti na kipindi cha awali.

 

Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Dkt. Rehema Nchimbi amesisitiza kwamba   kwa sasa Serikali imeweka  mikakati madhubuti ya kuufanya Mkoa wa Singida  kuwa miongoni mikoa itakayozalisha kwa  wingi mazao na  kuilisha Tanzania na nchi  mbalimbali za Afrika  na dunia kwa ujumla na hivyo kuwa na  Vyama vya Ushirika  makini ni jambo  lisiloepukika  kwenye Mkoa wa Singida.

“Tumeanza vizuri kwenye zao la Korosho na Alizeti sasa tunaongeza nguvu kufufua na kuanzisha mazao ya Mkonge na Parachichi” aliongeza Mhe. Nchimbi

Tuesday, November 10, 2020

TAKWIMU ZAIPAISHA TANZANIA UCHUMI WA KATI -SERIKALI

 


 A

A     Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Anjelina Lutambi (aliyesimama) akitoa ufafanuzi kwenye mkutano wa uelimishajiwa zoezi la ukusanyaji wa takwimu za mifugo,kilimo na uvuvi katika Kijiji cha  Msikii, Kata ya Muhamo, Mkoani Singida hivi karibuni(Pichana John Mapepele).

B

A.      Bibi Salma Mkumbo akiuliza swali kwa wataalamu kwenye mkutano wa uelimishaji wa zoezi la ukusanyaji wa takwimu za mifugo,kilimo na uvuvi katika Kijiji cha  Msikii, Kata yaMuhamo, Mkoani Singida hivi karibuni (Pichana John Mapepele).

c

A.      Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa (aliyesimama) akitoa ufafanuzikwenye mkutano wa uelimishaji wa zoezi la ukusanyaji wa takwimu za mifugo,kilimo na uvuvi katika Kijiji cha  Msikii, Kata yaMuhamo, Mkoani Singida hivi karibuni(Pichana John Mapepele).

DMeneja Takwimu Ofisi ya Taifa ya Takwimu Mkoa wa Singida, Naing’oya Kipuyo( aliyesimama) akitoa maelezo kwa  katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Anjelina Lutambi (mwenye miwani) na Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa (hayupo pichani) kwenye ofisi ya Serikali ya kijiji cha Msikii, Kata yaMuhamo, MkoaniSingidaHivikaribuni(Pichana John Mapepele).
E
Elibariki Musa, Mkazi wa kijiji cha Msikii Kata ya Muhamo, Mkoani Singida akiuliza swali kwa wataalamu  (Pichana John Mapepele)


Na John Mapepele, Singida 

Serikali imesema takwimu sahihi zilizokusanywa kutoka kwenye sekta mbalimbali za kimkakati za Mifugo, Kilimo na Uvuvi nchini zimeifanya Tanzania chini ya Uongozi wa Rais wa Awamu ya Tano Mheshimiwa John Pombe Magufuli kuingia kwenye Nchi za Uchumi wa Kati duniani.

Hayo yamesemwa hivi karibuni na ujumbe maalum wa kitaifa ulioongozwa na Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Anjelina Lutambi wakati  walipokuwa wanakagua zoezi la kitaifa ya ukusanyaji taarifa za kina za Kilimo, Mifugo, ufugaji wa samaki Mkoani Singida ambalo  limekamilika  hivi karibuni kwa mafanikio makubwa.

“Madhumuni makuu ya Sensa hii ni kupata taarifa muhimu za kilimo, mifugo na uvuvi zitakazotumika katika kupanga na kutathmini utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo ya sekta katika taifa la Tanzania, na endapo ukusanywaji wa takwimu utakuwa kwenye ubora unaositahili utasaidia kulifanya taifa kupea kwenye uchumi wa juu kabisa katika kipindi kifupi kijacho” ameongeza Dkt. Chuwa

 

Akifafanua amesema taarifa  kwa mfano za magonjwa ya mifugo na mazao zitaisaidia Serikali kuainisha maeneo yanayokabiliwa na visumbufu/magonjwa  ili kuchukua hatua stahiki na kupanga mipango ya kudhibiti.Pia taarifa kuhusu uzalishaji wa mazao zitasaidia kujua kiasi cha uzalishaji kwa maeneo husika na kuiwezesha Serikali kupanga upatikanaji wa masoko na uwezekano wa kuanzisha viwanda vya kusindika mazao hayo.

 

Aidha amesema taarifa kuhusu upatikanaji na matumizi ya ardhi zitatumika kupanga mipango ya matumizi bora ya ardhi vijijini  hivyo zitatumika kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji hapa nchini.

 

Dkt. Chuwa ameongeza kuwa matokeo ya Sensa ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi yanatarajiwa kuweka msingi imara wa sekta hii kwa miaka mingi iyajo, kwa  kuwa Sekta ya Kilimo ina umuhimu mkubwa  kwenye mustakabali wa maisha ya binadamu kwa kuwa ndiyo chanzo cha chakula na malighafi zinazohitajika katika viwanda hususani katika awamu hii inayoongozwa na dira ya uchumi wa viwanda.

 

“Kutokana na umuhimu huo, na kupitia Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia ya Mwaka 2030, Sekta ya Kilimo ilipewa Lengo la Pili  la Kutokomeza Njaa, Kuwa na Uhakika wa Chakula, Lishe Bora na Kukuza Kilimo Endelevu. Aidha, lengo hilo limesisitiza umuhimu wa kuongeza tija katika sekta ya kilimo kwa kuongeza thamani ya mazao na pia kusisitiza matumizi bora ya ardhi na kurutubisha udongo, ili kuongeza uwezo wa binadamu kukabiliana na kuhimili mabadiliko ya tabianchi na athari zake yakiwemo majanga mbalimbali kama mafuriko na ukame pamoja na majanga mengine ikiwemo ndege waharibifu” ameeleza Dkt. Chuwa

   

Dkt. Lutambi amesisitiza kuwa pamoja na faida za jumla ambazo mkulima atakazozipata Sensa hii itamsaidia mtu mmoja mmoja kutatua changamoto mbalimbali katika kilimo,mifugo na uvuvi hasa upatikanaji wa pembejeo, huduma za ugani, upatikanaji wa masoko kwa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi.

Ameongeza kuwa takwimu ni kitu cha msingi katika kupanga maendeleo kuanzia kwenye ngazi ya kijiji hadi taifa kwa kuwa zinasaidia kuonyesha changamoto na mafanikio na hivyo kusaidia kupata ufumbuzi wa kudumu wa changamoto hizo.

“Ni muhimu tukafahamu kuwa takwimu sahihi za mifugo, mazao na uvuvi zitasaidia  uchangiaji wa malighafi za  viwanda  vyetu hivyo kukuza uchumi wetu ambao tunautaka wa viwanda” amesisitiza Dkt. Lutambi

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Mohamed Bashe, kwenye hotuba yake, wakati  wa ufunguzi wa mafunzo ya wadadisi wa Sensa ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ya Mwaka wa Kilimo 2019/20, iliyofanyika katika Ukumbi wa TMDA,Mwanza Julai, 25 mwaka huu alisisitiza Mwaka huu 2020, Benki ya Dunia imeitangaza Tanzania kuwa katika kundi la nchi zenye uchumi wa kipato cha kati, ambapo alisema Taarifa hizi zimeleta faraja kubwa kwa sekta ya kilimo  kwa kuwa ndiyo iliyotoa mchango mkubwa zaidi katika Pato la Taifa wa asilimia 26.6 mwaka 2019 na pia inatoa ajira kwa takribani asilimia 66 ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi.

 

“Sekta ya kilimo ilichangia asilimia 24.3 ya mapato ya mauzo nje ya nchi mwaka 2019. Fedha hizi kwa kiasi kikubwa zinatumika nchini katika mambo mbalimbali ikiwemo ujenzi wa miundombinu wezeshi ya barabara, reli, maji, usambazaji umeme na kuimarisha miundombinu ya kutolea huduma za jamii kama vile afya na Elimu kwa lengo la kuimarisha maendeleo ya wananchi” alifafanua Dkt. Bashe

 

Aliongeza kuwa, kwa mujibu wa Ripoti ya Tathmini ya Umasikini Tanzania Bara ya Mwaka 2018, sekta hii ikiendelezwa vyema ndio pekee yenye uwezo wa kuleta maendeleo jumuishi nchini, hivyo  kuna umuhimu mkubwa wa zoezi la sensa ya mifugo, mazao na uvuvi likafanyika kwa ubora na kwa umakini  unaositahili.

 

Pia wakati wa tukio la uzinduzi wa mafunzo ya wadadisi wa Sensa hii, Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Amina Msengwa amesisitiza kuwa takwimu zina mchango mkubwa katika maandalizi na utekelezaji wa sera na mipango, na vile vile katika kufanya maamuzi sahihi yanayotakiwa kufikiwa kwa kutumia ushahidi stahiki (evidence based decision making).

 Amesema Sensa ya Mwaka wa Kilimo 2019/20, ni ya tano kufanyika hapa nchini tangu nchi ipate uhuru na inafanyika kwenye jumla ya maeneo yaliyochaguliwa ya kuhesabia2,820 ambapo kutokana na maeneo hayo kaya 33,807 kutoka Tanzania bara na Zanzibar.

Kwa upande wake, Meneja Takwimu Ofisi ya Taifa ya Takwimu Mkoa wa Singida, Naing’oya Kipuyo ameishukuru Serikali ya Mkoa wa Singida kwa kusaidia kufanikisha zoezi hili ambalo  limefanyika kwa takribani siku 50 ambapo pia amewapongeza wananchi kwa kutoa ushirikiano wa  kutosha.

 

 Kipuyo amesema taarifa zilizokusanywa kwenye Sensa hii ni za kipindi cha kuanzia tarehe 1 Oktoba, 2019 hadi tarehe 30 Septemba, 2020 na kuongeza kuwa Mkoa wa Singida umekamilisha zoezi hilo kwa maeneo yote ambapo maeneo madogo ya kuhesabia watu yaani Enumaration Areas (EA) 90 yenye kaya 1087 zilizochaguliwa kwa ajili ya kufanyiwa sensa hii zilifikiwa

Monday, November 9, 2020

WAFANYAKAZI WA BENKI YA I&M WAMEJITOLEA KUELIMISHA JAMII JUU YA MAMBO YA FEDHA NA UWEKAJI AKIBA KWA WANAWAKE NA VIJANA WAJASIRIAMALI

 

Timu ya wafanyakazi wa benki ya I&M waliovalia t-shirt za blue wakiwa katika picha ya pamoja na kikundi cha wanawake wajasiriamali kilichopo Yombo vituka walipoenda kutoa elimu ya bure kuhusu usimamizi wa fedha na ujasiriamali

Peter Joseph meneja msaidizi idara ya rasilimali watu akitoa elimu ya ujasiriamali kwa wanawake walioudhuria katika mafunzo hayo, Yombo jijini daresalaam.

Timu ya wafanyakazi wa benki ya I&M waliovalia t-shirt za blue wakiwa katika picha ya pamoja na kikundi cha wanawake wajasiriamali kilichopo Yombo vituka walipoenda kutoa elimu ya bure kuhusu usimamizi wa fedha na ujasiriamali

Mmoja wa wanawake walioudhuria katika mafunzo hayo, Bi. Eva Tumaini akizungumza na waandishi kuipongeza benki ya I&M kwa kutoa elimu ya fedha na ujasiriamali kwa jamii


Baadhi ya wafanyakazi wa benki ya I&M wakishirikiana na mmoja wa wanawake katika kufundisha mbinu za biashara ili kujikwamua kiuchumi kupitia mapishi.
 
                                                  ..................................................................
 


 Dar es salaam.

Benki ya I&M Tanzania yaanzisha mpango wa ‘IM FOR YOU’ ambao ni moja ya njia ya wafanyakazi wa benki hiyo kurudisha kwa jamii kwa kujitolea elimu bure kuhusu mambo mbalimbali ya kibenki ikiwemo maswala ya matumizi ya fedha, uwekaji akiba na ujasiriamali.

Siku ya Ijumaa Novemba 6, wafanyakazi wa Benki ya I&M wakiongozwa na Meneja Masoko na Mawasiliano ya Benki, Bi. Anitha Pallangyo, Meneja Msaidizi wa idara ya Rasilimali watu, Elimu na Maendeleo Bw. Peter Joseph, Bi. Hellen Mbwana kutoka idara ya ukaguzi wa ndani na wafanyakazi wengine waliotoka katika matawi ya hapa Dar es Salaam na idara nyingine mbalimbali ndani ya benki hiyo, walitembelea vikundi vya kina mama wajasiriamali wadogowadogo waliopo maeneo ya Yombo vituka jijini Dar es salaam, na kutoa elimu ya kuhusu mambo ya fedha, uwekaji akiba na ujasiriamali kwa wakina mama hao waliokusanyika kujipatia elimu hiyo.

Akielezea lengo la kuanzisha mpango huu wa ‘IM FOR YOU’ unaomaanisha ‘I&M Kwaajili yako’, wa kutoa elimu bure kwa jamii na lengo la kutembelea vikundi hivyo vya wakina mama vilivyopo maeneo ya Yombo Vituka, Bi. Anitha Pallangyo alisema, “Tumeazisha mpango huu kama moja ya njia ya kurudisha kwa jamii kile ambacho timu yetu ya rasilimali watu imekipata kutoka kwenye kazi zetu za kila siku, na kama tunavyojua kuwa elimu ni ufunguo wa maisha, hivyo tumeona ni vyema kukutana na vikundi mbalimbali vya wakina mama na vijana hasa ambao wanajishughulisha na biashara ndogondogo kujikwamua kiuchumi, ili kuwaongezea ujuzi na mbinu za kuongeza kipato. Mpango huu utasaidia hata serikali kupunguza idadi ya watu ambao hawajaajiriwa kwani unalenga kumfungua kijana na watanzania kwa ujumla kubuni mbinu mbalimbali za kibiashara ili kuweza kujiajiri.

Bw. Peter Joseph, Meneja Msaidizi idara ya rasilimali watu akiongea na waandishi katika tukio hilo alisema Benki ya I&M inajitahidi kuajiri wafanyakazi wenye uwezo mkubwa na ufanisi wa kazi, pamoja na kuwawezesha kuongeza ujuzi kupitia mafunzo mbalimbali ndani na nje ya ofisi hivyo imezalisha vijana wanaoweza kutoa elimu bora kwa jamii hasa kwa mambo ya fedha, umuhimu wa kujiwekea akiba na ujasiriamali.

Pamoja na kutoa elimu kwa jamii, timu hiyo ya wafanyakazi wa benki ya I&M ambayo ilienda kuwakilisha wafanyakazi wote kutoka idara mbalimbali, ilipeleka vitu mbalimbali ambavyo wafanyakazi walijitolea kwaajili ya kina mama wanaoishi kwenye mazingira magumu kama vile wajane, wamama wanaolea watoto yatima, na walemavu kwenye jamii hiyo, vitu hivyo ni pamoja na nguo, viatu, vyakula, sabuni, dawa za mswaki nakadhalka.

Benki ya I&M imekua mstari wa mbele katika kujitolea kwa jamii kupitia mikakati mbalimbali ya elimu, afya na mazingira. Benki hiyo inatoa huduma mbalimbali za kibenki kwa wananchi wote kwa ujumla ikiwemo akaunti za akiba za watoto, wanafunzi, wafanyabiashara, wanawake, mikopo, huduma za kuhamisha fedha, huduma za kubadili fedha za kigeni nakadhalika.  Benki hiyo inatarajia kuanzisha huduma za WAKALA hivi karibuni ambapo inategemea kuwa na  mawakala walioenea Dar es salaam na mikoani, pia ina matawi yanaoendelea kutoa huduma bora ambayo ni;Tawi la maktaba, tawi kuu linalo patikana mtaa wa Indira Gandhi, Kariakoo, Nyerere, Oysterbay, Moshi, Arusha na Mwanza. Pia kupitia huduma zake za benki kwa njia ya simu (Mobile Banking) *150*32#, kwa njia ya mtandao (Internet Banking) na App, wateja wake wanaweza kupata huduma za kibenki  saa 24 mahali popote wowote